FM Manyara
FM Manyara
29 May 2026, 2:25 pm

Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara imetoa hukumu ya miaka 20 kwa aliyekuwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ruvu Remit Godbless Felix Mollel kwa makosa ya uhujumu uchumi katika shauri la uhujumu uchumi namba 22415/2025.
Na Mzidalfa Zaid
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa Wilaya ya Simanjiro Onesmo Nicodemos ambapo imeelezwa mshtakiwa alishtakiwa kwa makosa ya ufujaji na ubadhirifu kinyume na K/f cha 28(1) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329.
Shauri hilo limeendeshwa Mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Wakili Faustin Mushi
Mshtakiwa ametiwa hatiani na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka ishirini (20)gerezani kwa kosa la kwanza la ufujaji na ubadhirifu na katika kosa la pili la wizi akiwa mtumishi wa umma, mshtakiwa ametiwa hatia na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha mwaka mmoja (1) gerezani.
Aidha mshtakiwa ameamriwa kurejesha kiasi cha shilingi 3,300,000 alichokifanya ubadhirifu katika akaunti ya benki ya Maendeleo ya Kijiji cha Ruvu Remit.