FM Manyara
FM Manyara
23 July 2026, 4:24 pm

Wananchi mkoani Manyara wamehimizwa kujiunga na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Tanzania Red Cross Society – TRCS) ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na chama hicho, ikiwemo mafunzo ya huduma ya kwanza, shughuli za kujitolea, pamoja na kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya kibinadamu na maendeleo ya jamii.
Na Mzidalfa Zaid
Wito huo umetolewa leo na Mratibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Manyara, Mohamed Hamad, wakati akizungumza na FM Manyara. Amesema kuwa jukumu kuu la TRCS ni kutoa huduma za kibinadamu bila ubaguzi, kuwahudumia waathirika wa majanga, kushiriki katika shughuli za uokoaji wakati wa dharura, pamoja na kuwajengea uwezo vijana na jamii kupitia programu mbalimbali za kujitolea.
Ameeleza kuwa uanachama wa Red Cross unawapa wananchi nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kuokoa maisha, kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga na kuchangia maendeleo ya kijamii kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na chama hicho kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania Mkoa wa Manyara, Bi. Tausi Khalfan, amesema katika kipindi chake cha uongozi cha miaka mitano atajikita katika kuongeza idadi ya wanachama, kuimarisha matawi ya chama katika wilaya zote za mkoa huo, pamoja na kuhamasisha ushiriki mpana wa wananchi katika shughuli za kibinadamu.
Amesema uongozi wake pia utaweka msisitizo katika kuwajengea uwezo vijana na wajitolea, kuimarisha ushirikiano na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo, na kuhakikisha Red Cross Mkoa wa Manyara inaendelea kuwa chombo madhubuti cha kutoa huduma za kibinadamu na kuwafikia wananchi wenye uhitaji kwa wakati.
Bi Tausi amewahimiza wananchi kujiunga na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania ili kwa pamoja kujenga jamii yenye mshikamano, ustahimilivu na uwezo wa kukabiliana na majanga na changamoto mbalimbali za kibinadamu.