FM Manyara

TAKUKURU rafiki yawafikia wananchi GIDAS

14 October 2026, 6:52 pm

Picha ya baadhi ya wananchi wa kata ya Gidas wakipata elimu kutoka TAKUKURU

TAKUKURU rafiki yafika katika kata ya Gidas na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu elimu ya madhara ya rushwa.

Na Mzidalfa Zaid

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara kupitia programu ya TAKUKURU Rafiki imekutana na wananchi wa Kijiji cha Endadimet, Kata ya Gidas wilayani Babati, kwa lengo la kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa kero zinazoweza kuchochea vitendo vya rushwa katika jamii.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Dawati la Uzuiaji Rushwa TAKUKURU mkoa wa Manyara Paschal Muhagama, ametoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kubaini na kuwasilisha kero zinazohusiana na huduma mbalimbali za kijamii ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.

Aidha, programu ya TAKUKURU Rafiki inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi ambao ni wanufaika wa huduma na watoa huduma katika ngazi za vijiji na kata, hatua inayosaidia kubaini changamoto zinazoweza kutoa mwanya wa vitendo vya rushwa.

Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Gidas akiwemo  Kaim mtendaji wa Kijiji Baraka Malle wamewapongeza maafisa wa TAKUKURU kwa kuwafikia kupitia programu hiyo, wakisema imewapa fursa ya kueleza kero zinazowakabili na kuomba taasisi hiyo kuendelea kuwatembelea ili kuimarisha elimu na juhudi za kuzuia rushwa katika jamii.