FM Manyara
FM Manyara
2 November 2026, 1:21 pm

Katika kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka na kuanza kwa mwaka mpya, Watanzania pamoja na raia wa kigeni wametakiwa kutumia kipindi hicho kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ili kujionea rasilimali za utalii zilizopo nchini.
Na Mzidalfa Zaid
Wananchi wametakiwa kutumia muda wa sikukuu za mwisho wa mwaka kutembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi na vivutio vya utalii vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), ili kujifunza na kujionea utajiri wa rasilimali za wanyamapori na mazingira ya asili yaliyopo nchini.
Wito huo umetolewa na Afisa Mhifadhi kutoka TAWA Kanda ya Kaskazini, Rahel Nkuni wakati akiongea na Fm Manyara amesema utalii una faida mbalimbali kwa wananchi ikiwemo kupata fursa ya kujionea wanyamapori wa aina tofauti pamoja na ndege wanaopatikana katika maeneo hayo.
Amesema mbali na kujionea vivutio vya asili, utalii pia unasaidia watu kupata burudani, kufurahia mazingira ya asili na kupunguza msongo wa mawazo unaoweza kusababishwa na shughuli mbalimbali za kila siku.
Aidha katika hatua nyingine, Nkuni amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira na wanyamapori kwa kuepuka shughuli zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira au kuhatarisha maisha ya wanyamapori, akisisitiza kuwa uhifadhi ni jukumu la kila mmoja.