Bufadeso yakabidhi miche ya miti 500 mtaa wa Main Bunda
6 November 2024, 9:03 pm
Shirika la Bufadeso linatoa miche ya miti bure kwa taasisi ambazo zinatoa huduma kwa watu kama vile shule, vituo vya kutolea huduma za afya miongoni mwa taasisi zingine.
Na Adelinus Banenwa
Wakazi wa mtaa wa Maini kata ya Kabasa Halmashauri ya Mji wa Bunda wamelishukuru shirika la Bufadeso kwa kuwapatia miche ya miti 500 kwa ajili ya kupandwa kwenye eneo la zahanati ya mtaa huo
Wakizungumza wakati wa upokeaji wa miti hiyo wananchi hao wamesema walituma maombi kwa shirika hilo ili kuwapatia miti kutokana na eneo la zahanati hiyo ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi wakiungwa mkono na serikali lilikuwa wazi sana kutokana na kukosa eneo la kivuli ambacho pindi zahanati hiyo itakapokamilika wagonjwa watakosa sehemu ya kupumzika.
Kwa upande wake mwenyekiti wa shirika la Bufadeso Maziba Agustini amesema shirika hilo baada ya kupokea maombi kutoka kwa wakazi wa maini wao kama shirika wametoa miche ya miti 500 ambayo ipo katika Nyanja kuu tatu ikiwa ni miche ya matunda , mbao pamoja na vivuli.
Aidha mwenyekiti huyo amesema shirika la Bufadeso linatoa miche ya miti bure kwa taasisi ambazo zinatoa huduma kwa watu kama vile shule, vituo vya kutolea huduma za afya miongoni mwa taasisi zingine.
Aidha ametoa wito kwa wananchi wa mtaa wa Main kuhakikisha miche hiyo wanaitunza ili iweze kustawi na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yaaweza kutokea katika eneo hilo la zahanati kama vile athari za upepo, na mmomonyoko wa udongo,
Dickison Juma Mbogo mtendaji wa mtaa wa Main amehaidi kuilinda na kuitunza miti hiyo kwa kushirikiana na viongozi wenzake ili kusudi la shirika la Bufadeso la kutunza mazingira kupitia miti liweze kufanikiwa lakini pia wananchi waweze kunufaika na uwepo wa miti hiyo katika zahanati yao.