Mazingira FM

Serengeti: kituo cha taarifa na maarifa Nyambureti waadhimisha siku 16 za kupinga ukatili

7 December 2022, 8:11 pm

 

Ushirikiano hafifu wa jamii na kuwa mbali na vyombo vya dola kama kituo cha polisi ni moja kati ya changamoto zinazokwamisha juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika kata ya Nyambureti Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Haya yamebainishwa leo wakati wa Maadhimisho ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyofanywa na Kituo cha Taarifa na Maarifa KC kata ya Nyambureti katika viwanja vya Sokoni kijiji cha Maburi Wilaya ya Serengeti.

Katika risala hiyo iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyambureti, Peter Bachuta imebainisha mafanikio mbalimbali yaliyofanywa na kituo cha Taarifa na Maarifa katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia huku wakibainisha masuala mbalimbali yanayokwamisha juhudi hizo.

Akijibu risala hiyo Mh Peter Bachuta amesema ni kweli kumekuwa na ushirikiano mdogo kutoka kwa jamii pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wanakwepa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria jambo linalopelekea ukatili kuongezeka kwa jamii.

Maadhimisho ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Weka Rasilimali Kuongeza Ushiriki wa Wanawake”