”Wakazi wa Bunda ombeni kuunganishiwa maji ili mabomba yasipasuke”
12 November 2023, 12:27 pm
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bunda Ndg. Mayaya Abraham Magesse amewasihi wakazi wa Bunda kuomba kuunganishiwa maji kwenye makazi yao kutoka Mamlaka ya Maji Bunda.
Na Adelinus Banenwa
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bunda Ndug. Mayaya Abraham Magesse amewasihi wakazi wa Bunda kuomba kuunganishiwa maji kwenye makazi yao kutoka Mamlaka ya Maji Bunda kwa kuwa mamlaka hiyo kwa sasa inazalisha maji ya kutosha.
kauli hiyo ameitoa katika ziara ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa na BUWSSA ndani ya mji wa Bunda.
Awali akitoa ufafanuzi kuhusu hoja ya kupasuka kwa mabomba mara kwa mara mkurugenzi wa BUWSSA Bi Esther Giryoma amesema tatizo siyo ubora wa mabomba yaliyopo bali ni msukumo mkubwa wa maji uliopo kwa sasa huku akitaja changamoto ya idadi ndogo ya watumiaji maji ukilinganisha na maji yanayozalishwa.
ziara hiyo imehusisha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Bunda, Bodi ya mamlaka ya maji Bunda, pamoja na ofisi ya chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Bunda.
Aidha katika ziara hiyo imekaguliwa miradi mitatu ikiwa ni pamoja na mradi wa Manyamanyama, Mugaja unaogharimu shilingi 1.1 bilion ambao ukikamilika utawanufaisha zaidi ya wakazi elfu tano, pamoja na mradi wa Balili, Rubana na Kunzungu unaogharimu zaidi ya shilingi 700 milion.