Baraka FM
Baraka FM
1 October 2026, 14:14

Dkt. Raymond Mgeni akizungumza na waandishi wa habari mkoa wa Mbeya(picha na Josea Sinkala)
Kutokana na uwepo wa ongezeko kubwa la watu kukubwa na changamoto ya afya ya akili jamii imehimizwa kufanya vipimo mara kwa mara ili kufahamu mwenendo wa afya zao.
Na Josea Sinkala
Waandishi wa habari wametakiwa kuzingatia weledi, maadili, kanuni na sheria zinazowaongoza katika kutekeleza majukumu yao, ili kuepuka migogoro inayoweza kuzuka katika jamii, ikiwemo kuchochea chuki,huku wakitunza afya zao za akili ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Wito huo umetolewa wakati Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ukiendesha mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu afya ya akili na usalama wanapokuwa kazini.
Akitoa elimu hiyo kwa wanahabari mkoani Mbeya, Dkt. Raymond Mgeni, daktari kutoka Kitengo cha Afya ya Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya,amewashauri waandishi wa habari wanapokumbana na changamoto mbalimbali, wanapaswa kutafuta njia sahihi za kuzitatua kwa utulivu na kuepuka kuchukua hatua zinazoweza kuhatarisha afya zao za akili au usalama wao.
Kwa upande wake, mkufunzi wa mafunzo ya usalama kwa waandishi wa habari kutoka Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Gabriel Mbwile, amesisitiza umuhimu wa wanahabari kuzingatia maadili, weledi na kanuni za kazi, huku wakitanguliza usalama wao wanapotekeleza majukumu.
Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo, akiwemo Josephat Semba na Marygoreth Mpepo, wamesema mafunzo hayo yamewajengea uelewa na yatawasaidia kutambua umuhimu wa kutunza afya zao za akili.
Wamesema pia elimu hiyo itawasaidia kutumia njia sahihi wanapokabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kushughulika na watu wenye changamoto za afya ya akili, msongo wa mawazo au sonona.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutambua na kuthamini usalama wao, pamoja na kuongeza uelewa kuhusu afya ya akili, changamoto za afya ya akili na magonjwa ya akili.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa usalama na weledi, huku wakichangia kupunguza migogoro na kujenga jamii yenye uelewa zaidi kuhusu afya ya akili na usalama.