Baraka FM

Mume aua mke kwa kutenganisha kichwa na kiwiliwili Igurusi Mbeya

14 March 2024, 14:13

Mwanaume mmoja katika eneo la Igurusi wilayani Mbarali mkoani Mbeya amejichukulia hatua mkononi kwa kumchinja mke wake mithiri ya kuku na kumtenganisha kichwa na kiwiliwili.

Na Ezekiel Kamanga

Simanzi na vilio vimetawala kwa wakazi wa kitongoji cha Masista kijiji cha Lusese kata ya Igurusi baada ya Ombeni Kilawa mkazi wa kijiji hicho wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kumuua mke wake  Happiness Mwinuka kwa kumchinja  na kutenganisha kichwa na kiwiliwili.

Tukio hilo limetokea majira ya  saa 7.00 usiku wa kuamkia  Machi 13, 2024 ambapo jirani amesema alisikia kelele za watu wakigombana lakini baada ya nusu saa kukawa kimya hivyo kuamua kupiga yowe ndipo watu walipojitokeza na askari polisi kufika kisha kubomoa mlango wa chumbani kwao na baada ya kuingia  Kilawa alikuwa ameshatekeleza mauaji kwa kumchinja mke wake na kwa kutenganisha kichwa na kiwiliwili.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa mgogoro wa ndoa ambapo walitengana miaka mitatu iliyopita na mwanaume kuacha mji ambapo ndugu wamejaribu kusuluhisha ili mumewe arejee lakini mkewe hakuwa tayari.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia kwa kamanda ACP Benjamin Kuzaga limethibitisha  kumshikilia Ombeni Manase Kilawa [43] mkazi wa Lusese wilaya ya Mbarali anayetuhumiwa kumuua mke wake aitwaye Happiness Gervas Mwinuka [40] mkazi wa kijiji cha Lusese kwa kumkata na kitu chenye ncha kali.

Aidha Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya, linatoa wito kwa jamii kuwa pindi wanapopatwa na tatizo au changamoto katika ndoa zao isiwe suluhisho lake kujichukulia sheria mkononi bali ni kutafuta ushauri kwa wazazi, walezi, wasimamizi wa ndoa, viongozi wa dini, madawati ya jinsia na watoto waliopo kila Wilaya ya Kipolisi, katika ofisi za halmashauri au kutafuta haki kwenye mahakama ili kuepuka madhara.