Baraka FM

Iringa watoa msaada wa tsh. 42,944,000  kwa waathirika mafuriko Hanang

19 December 2023, 19:23

Na Moses Mbwambo

Mkuu wa mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego akiwa ameambatana na viongozi wa Mbalimbali wa mkoa huo wakiwemo wakuu wa Wilaya Wakurugenzi viongozi wa Chama cha Mapinduzi na kamati ya ulinzi wametoa Mkono wa pole kwa Waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Hanang mkoa wa Manyara

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Iringa Mhe. Dendego ametoa salamu za pole kwa waathirika wote na kwa wale wote walioondokewa na ndugu jamaa pamoja na marafiki na kuwataka Watanzania kuendelea kujitokeza kuendelea kutoa misaada katika eneo hilo.

Nae mkuu wa Wilaya ya Hanang Mhe. Janeth Mayanja ametoa shukrani nyingi sana kwa serikali kwa kuwa karibu nao katika nyakati zote pia kwa  Wananchi wa Mkoa wa Iringa na Watanzania kwa ujumla kwa Moyo wao wa upendo kwani toka tukio hilo lilipotokea ni watu wengi wamejitokeza  kwa kutoa pole na kutoa misaada.

Wakiwa katika wilaya hiyo wametembelea katika maeneo yaliyoathiriwa na kujionea hali ilivyo kwa sasa huku wakipongeza kazi kubwa inayoendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha hali inakuwa shwari kama hapo awali.

Msaada uliotolewa na mkoa wa Iringa ni chumvi, mahindi,ndoo za maji,mchele,mashuka,unga, magodoro,mkaa mweupe, na milunda ya miti ambapo msaada huu una thamani ya Tsh. 42,944,000.