Baraka FM

Ujenzi Stendi ya Chimbuya Songwe kukamilika mwezi mei 2024

24 March 2024, 09:04

Ujenzi wa stendi chimbuya ukiendelea (picha na Ezra Mwilwa)

Baada ya kilio cha stendi ya kuegesha magari ya mizigo songwe hatimaye swala hilo limepatiwa ufumbuzi

Na Ezra Mwilwa

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga amesema Matengenezo ya mahali pa kuegesha malori eneo la Chimbuya, Mbozi, Mkoani Songwe yatakamilika Mei mwaka huu.

Mhandisi Bishanga amesema Serikali imetenga Sh bilioni 1.8 kwa matengenezo ya awamu ya kwanza ambayo yanaendelea sasa.

Amesema matengenezo ya awamu ya kwanza yanahusu utengenezaji wa sakafu ngumu ambayo itahimili malori yenye uzito wa aina yoyote na pia utajengwa wigo kuzunguka eneo lote.

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa eneo la kuegesha magari ya mizigo Chimbuya Songwe (picha na Ezra Mwilwa)

Mhandisi Bishanga amesema eneo linalotengenezwa sasa litakuwa na uwezo wa kupokea malori 200 na lengo la Serikali ni kulifanya eneo hilo kuwa huduma zote muhimu zikiwamo za gereji, hoteli na nyumba za kulala wafanyakazi wa malori.

Mhandisi Bishanga amewapongeza wananchi wa Mbozi hususani wa Chimbuya kwa jinsi wanavyotoa ushirikiano kwa Serikali na kwamba ujenzi wa kituo cha malori ni fursa kwao kwa masuala ya biashara.