Baraka FM

Aliyeua watoto wake wawili kwa sumu mkoani Mbeya naye afariki

12 March 2024, 20:55

Kamanda wapolisi mkoa wa Mbeya ACP Benjamini Kuzaga(picha na mtandao)

Siku zote wanasema uchungu wa mwana aujuaye mzazi ,hii imekuwa tofauti kwa mwanamke mmoja mkoani Mbeya kuchukua maamzi ya kuwanywesha watoto wake sumu na kusababisha kifo.

Na Hobokela Lwinga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa taarifa kuwa mtuhumiwa Dainess Paul Mwashambo [30] mkazi wa kijiji cha Mashese aliyekuwa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya amefariki.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi mkoa wa Mbeya kupitia kwa kamanda wa jeshi ACP Benjamin Kuzaga inaeleza kuwa mtuhumiwa huyo alifariki dunia tarehe 09 Machi, 2024 majira ya saa 10:15 jioni.

Awali Machi 05, 2024 mtuhumiwa Dainess Paul Mwashambo [30] akiwa nyumbani kwake kijiji cha Mashese kata ya Ilungu halmashauri ya Mbeya aliwanywesha sumu ya kuulia magugu aina ya “Pare Force” watoto wake wawili na kusababisha vifo vyao na kisha na yeye alikunywa sumu hiyo iliyopelekea kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kwa matibabu.

Mtuhumiwa aliendelea kupatiwa matibabu Hospitalini hapo lakini tarehe 09 Machi, 2024 alifariki duniani.