Baraka FM

Serikali yajipanga kutatua changamoto ya maji mkoani Songwe

28 November 2023, 16:25

Na Hobokela Lwinga

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi,amesema kuwa serikali inatekeleza miradi nane yenye thamani ya sh. Bilioni 13.3 kwa ajili kutoa huduma ya maji kwenye Vijiji 22 katika Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe.

Mhandisi Mahundi ameeleza hayo leo Novemba 24, 2023, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Wilayani Mbozi, Waziri Mkuu yupo katika ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Songwe.

Alisema kuwa jumla ya vijiji 99 vimepatiwa huduma ya maji kati ya Vijiji 121 vilivyopo wilayani Mbozi.

Aliongeza kwa kusema kuwa serikali inaendelea na jitihada za kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji katika miji ya Vwawa na Mlowo wilayani mbozi kupitia mradi wa ukarabati wa chanzo cha maji Mwansyania na upanuzi wa mtandao wa maji wenye Jumla ya thamani ya sh. bilioni 3.9.

Aidha, Mhandisi Mahundi alisema mbali na jitihada hizo, serikali ipo kwenye mchakato wa utekelezaji wa mradi wa maji kwa kutumia chanzo cha maji cha mto Momba ambao unagharimu kiasi cha sh. bilioni 340 kwa ajili ya kutatua kero ya maji katika miji ya Tunduma, wilayani Momba pamoja na miji ya Vwawa na Mlowo, wilayani Mbozi.