Baraka FM

Rc Songwe awapongeza walimu

27 February 2024, 19:56

Na mwandishi wetu, Songwe

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Dkt. Francis K. Michael, ametembelea na kukagua hali ya ufundishaji na ujifunzaji katika Shule ya Msingi Katete iliyopo Kata ya Mpemba na Shule ya Msingi Mpemba iliyopo Kata ya Katete katika Halmashauri ya Mji Tunduma.

Dkt. Michael, amewapongeza Walimu kwa jitihada kubwa ya kuwafundisha Wanafunzi ambao ametoa rai kwa Walimu wote katika Halmashauri hiyo kuongeza bidii na maarifa katika utendaji wao wa kazi ili kusiwepo na Wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kwani kwa kufanya hivyo ufaulu utaongezeka na jamii itakombolewa.

Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo amesema zoezi la kutembelea shule za msingi litakuwa endelevu na ataendelea kulifanya kwa kustukiza hivyo amewataka Walimu kutimiza wajibu wao ipasavyo maana hawatajua saa na muda atakaofika katika shule zao.