Baraka FM

Serikali yatoa zaidi ya Tsh. 87 mil kwa vikundi vya vijana bodaboda Kyela

13 July 2026, 23:33

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Nanauka baada ya kukabidhi mkopo kwa vijana (picha na Hobokela Lwinga)

Vijana wanapaswa kutumia mikopo ya serikali kujiajiri kwa sababu inawapa mtaji wa kuanzisha au kupanua biashara zao. Kujiajiri husaidia kupunguza ukosefu wa ajira, kuongeza kipato, na kuboresha maisha ya vijana pamoja na familia zao.

Na Hobokela Lwinga,Kyela Mbeya

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 87 kwa vikundi viwili vya vijana 22 wanaojishughulisha na usafirishaji wa abiria kwa pikipiki (bodaboda) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha vijana kiuchumi.

‎‎Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikopo hiyo, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Nanauka, amesema vikundi vilivyonufaika ni Muungano chenye wanufaika sita na Safari na Usalama Bodaboda Njisi chenye wanufaika 16.‎‎

Dkt. Nanauka amewataka vijana waliopata mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuboresha maisha yao na kukuza shughuli zao za kiuchumi. Alisisitiza kuwa hawapaswi kutumia pikipiki hizo kwa vitendo vya uhalifu wala kuziuza, kwani kufanya hivyo kunakiuka masharti ya mkopo na kunadhoofisha juhudi za Serikali za kuwawezesha vijana.‎‎

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Nanauka(picha na Hobokela Lwinga)

Awali, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mbeya, Selina Mtenya akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa amesema Serikali ina jukumu la kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana nchini.Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Mkoa wa Mbeya ulifanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6.6 kwa makundi mbalimbali ya vijana.

Baadhi ya wananchi wakishuhudia utoaji mikopo kwa vijana (picha na Hobokela Lwinga)

‎‎Kwa upande wao, Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase, na Mbunge wa Kyela, Baraka Mwamengo, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuipa kipaumbele wilaya hiyo katika utoaji wa mikopo ya maendeleo. Viongozi hao wamewasihi vijana kutumia ipasavyo fursa waliyoipata ili kujikwamua kiuchumi na kuongeza ajira.‎‎

Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase(picha na Hobokela Lwinga)

Naye Meneja wa Benki ya CRDB, Tuty Harison, ambaye benki yake inasimamia utoaji wa mikopo hiyo amewahimiza vijana kutokuwa na hofu ya kukopa kwa ajili ya maendeleo akieleza kuwa mikopo hiyo ni fursa ya kukuza biashara na shughuli za uzalishaji. Amewahakikishia kuwa fedha za kutosha zimetengwa kwa ajili ya fursa za kuwawezesha vijana wenye sifa.‎‎

Baadhi ya wanufaika wa mkopo huo walisema maisha yao yameanza kubadilika baada ya kupata uwezeshaji huo. Walieleza kuwa kabla ya mkopo walikuwa wakikabiliwa na changamoto za kipato na maisha duni, lakini sasa wana matumaini ya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kuboresha maisha ya familia zao.