Baraka FM

Chunya wafurahia semina ya udiakonia,wasisitizwa kujali watu wenye mahitaji

21 April 2026, 20:46

Baadhi ya washiriki wa semina katika wilaya ya Chunya (picha na Hobokela Lwinga)

Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi kupitia Idara ya Udiakonia imeendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kutoa huduma za udiakonia kwenye maeneo yao ya kazi ya Mungu.

Na Hobokela Lwinga

Idara ya Udiakonia ya Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi, imeandaa semina maalum kwa watumishi wa kanisa wakiwemo wachungaji, mawakili, Viongozi wa mipango,uchumi na maendeleo,pamoja na viongozi wa udiakonia kutoka Wilaya ya Chunya.

‎Semina hiyo imefanyika katika Ushirika wa Kiwanja, Wilaya ya Chunya, na kuhudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa KMT–JKM, Mchungaji Agnes Njeyo, pamoja na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo inayoongozwa na Mchungaji Nuru Mwamahonje.

Mchungaji Agnes Njeyo makamu mwenyekiti KMT-JKM(kushoto) katikati ni Katibu idara ya udiakonia KMT-JKM Eliudy Mahenge (kulia) ni Emmanuel Angetile afisa afya wa idara(picha na Hobokela Lwinga)

‎Akifungua semina hiyo, Mchungaji Agnes Njeyo makamu mwenyekiti KMT-JKM amewahimiza washiriki kumtanguliza Mungu katika huduma zao, sambamba na kuonesha upendo kwa jamii inayowazunguka,Amesisitiza kuwa huduma ya kweli inapaswa kuakisi maadili ya Kikristo yanayojengwa juu ya imani na matendo mema.

Mchungaji Agnes Njeyo makamu mwenyekiti KMT-JKM (picha na Hobokela Lwinga)

Kwa upande wake, Katibu wa Idara ya Udiakonia Jimbo la Kusini Magharibi, ndugu Eliudy Mahenge, ameeleza kuwa udiakonia ni msingi wa matendo ya Yesu Kristo, unaojikita katika upendo, huruma na kujitoa kwa ajili ya wengine.

Katibu wa Idara ya Udiakonia Jimbo la Kusini Magharibi, ndugu Eliudy Mahenge(picha na Hobokela Lwinga)

‎Naye Afisa Afya wa Idara ya Udiakonia KMT–JKM, Emmanuel Angetile, amebainisha kuwa katika utekelezaji wa udiakonia, jamii inapaswa kuwajali watu wenye ulemavu, kwani wana haki sawa na wanastahili kushirikishwa kikamilifu katika shughuli za kijamii.

Afisa Afya wa Idara ya Udiakonia KMT–JKM, Emmanuel Angetile(picha na Hobokela Lwinga)

‎Aidha, Mwenyekiti wa KMT–JKM Wilaya ya Chunya, Mchungaji Nuru Mwamahonje, amewataka washiriki kuwa na ari ya kujifunza mambo mbalimbali yatakayowasaidia kuboresha huduma zao na maisha kwa ujumla.

Mwenyekiti wa KMT–JKM Wilaya ya Chunya, Mchungaji Nuru Mwamahonje(picha na Hobokela Lwinga)

‎Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wamelishukuru kanisa kupitia Idara ya Udiakonia kwa kuandaa mafunzo hayo, huku wakihimiza kuongezwa kwa uwekezaji zaidi katika kuwajengea uwezo watumishi wa kanisa ili kuimarisha utendaji wa shirika.

Baadhi ya washiriki wa semina katika wilaya ya Chunya (picha na Hobokela Lwinga)