Baraka FM

Kamati zote zijengewe uwezo usimamizi miradi

30 January 2024, 17:38

Na mwandishi wetu

Mkuu wa wilaya ya Chunya Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Mhe. Mbaraka Alhaji Batenga ameagiza kamati zote za ujenzi zinazosimamamia Miradi mbalimbali ya Ujenzi wilayani Chunya zijengewe uwezo wa kusimamia miradi husika ili watakapokiuka maelekezo waweze kuchukuliwa hatua kwa haki kwa mujibu wa Kanuni, Taratibu na Miongozo

Ametoa agizo hilo jana tarehe 29/1/2024 wakati alipofanya ziara ya kukagua mradi wa Zahanati ya Igundu ambapo Zaidi ya milioni hamsini (50,000,000) zimepelekwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwepo tanki la maji, vinawia mikono, vyoo na kichomea taka

“Wajumbe wote wa kamati za ujenzi wajengewe uwezo wa kusimamia miradi hiyo kabla ya kukabidhiwa jukumu la kuanza kusimamia mradi husika jambo ambalo litasaidia wajumbe hao kusimamia ipasavyo mradi husika na hata kuhakikisha ukamilifu wa mradi huo” alisema Mhe.Batenga

Aidha Mhe Batenga ameuagiza uongozi wa Afya kuzingatia ushauri uliotolewa na Wakala wa maji na Usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) pamoja na TANESCO ili kuhakikisha wananchi wa Igundu wanaendelee kutatua changamoto zote maana hilo ndio lengo la Serikali kusogeza miradi mbalimbali kwa wananchi wake wakiwepo wananchi wa wilaya ya Chunya

Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Kaimu Mganga Mkuu Edward Tengulaga alisema siku saba zinatosha kuhakikisha kibao kinachoonesha huduma zinazotolewa katika zahanati hiyo kinawekwa pamoja na kibao kinachoonesha uwepo wa Zahanati eneo hilo vitu ambavyo vilibainishwa kwamba ni muhimu na havikuwepo ili kuwarahishisia wananchi ambao sio wenyeji watakapohitaji huduma hiyo

Ziara ya Mkuu wa wilaya ililenga kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika kata ya Sangambi ambapo alitembelea pia mradi wa Maji Igundu, mradi wa ujenzi wa vyoo katika Shule ya msingi Sangambi, mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya pamoja na kukagua hali ya mazingira katika kitongoji cha Tukuyu.