Baraka FM

Epukeni kutenda uhalifu

28 December 2023, 18:24

Na mwandishi wetu,Songwe

Waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Thomas Jimbo Kuu la Mbeya wametakiwa kuzishinda dhamiri zao mbaya ili kutotenda matendo uhalifu katika jamii.

Hayo yalisemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya, wakati aliposhiriki ibada hiyo ya misa takatifu na kutoa elimu kwa waumini walioshiriki ibada hiyo kuhusu madhara ya kutekeleza dhamiri mbaya akiwa anasisitiza mahubiri ya Padre Karolo Kavindi wa Parokia hiyo ambayo inapelekea kufanya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto.

Kamanda Mallya alisema si jambo jema kwa muumini anayekuja kanisani kumcha Mumgu lakini anatekeleza dhamiri mbaya ambayo inampelekea kufanya ukatili na vitendo vya uhalifu.

Kamanda Mallya aliongeza kuwa kumcha Mungu ni kuyatenda yale yote aliyoyaelekeza katika biblia na vitabu vitakatifu pia kuyaishi ili kutokomeza vitendo viovu katika jamii na hapo tutakuwa tumeishinda dhamiri mbaya ndani ya mioyo yetu.