Baraka FM
Baraka FM
20 April 2026, 22:21

Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi limeendelea kuboresha ofisi zake ikiwa ni kuweka mazingira Rafiki ya ufanyaji kazi ya Mungu.
Na Hobokela Lwinga
Wilaya ya Mbarali Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, imezindua rasmi harambee ya ujenzi kwa ajili ya upauaji wa ofisi za wilaya hiyo.
Ibada ya uzinduzi wa harambee hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika Kanisa la Moravian Ushirika wa Igurusi, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kanisa pamoja na serikali. Katika harambee hiyo,kila Mkristo ndani ya wilaya ya Mbarali anahimizwa kuchangia debe moja la mpunga ili kufanikisha zoezi hilo.

Akifungua ibada hiyo kwa niaba ya Askofu wa kanisa la Moravian Jimbo la kusini magharibi Robert Pangani, Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Wilaya ya Mbarali, Mchungaji Paul Mwampamba,aliwataka waumini kutambua wajibu wao wa kutoa sadaka kwa ajili ya ujenzi, ili kuendeleza kazi ya Mungu katika wilaya hiyo.

Aidha, Mchungaji Mwampamba amesisitiza kuwa ujenzi wa ofisi hizo hautakuwa na manufaa kwa waumini wa Moravian pekee, bali utahudumia jamii nzima ya Mbarali.
Katika hatua nyingine, ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano unaoendelea kuitoa kwa kanisa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Katibu wa wilaya ya Mbarali Mchungaji Laida Msangawale ameeleza kuwa hadi sasa ujenzi huo umefikia hatua ya lenta, ukiwa umegharimu kiasi cha shilingi milioni 50. Aliongeza kuwa wilaya inalenga kukusanya jumla ya shilingi milioni 100 ifikapo tarehe 7 Juni, 2026.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa ya Ujenzi amewahimiza waumini kutotegemea wengine katika zoezi hilo, bali kila mmoja achukue jukumu la kuchangia ili kujenga historia ya kukumbukwa katika kulijenga kanisa la Mungu.

Katika hafla hiyo, mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Mhe. Twalibu Lubandamo, alichangia shilingi milioni 10 kuunga mkono juhudi za ujenzi huo huku akisema taasisi za dini zimekuwa na mchango mkubwa wa kuhamasisha Amani nchini.

Harambee hiyo inaendeshwa chini ya kauli mbiu isemayo:“Debe langu moja la mpunga litapaua jengo letu.”