Baraka FM
Baraka FM
6 June 2024, 17:11

Jiji la Mbeya likiwa bado kwenye majonzi makubwa ya kutokea ajali eneo la Mbembela huku wananchi na ndugu marehemu wakiendelea kuitambua miili ya wapendwa wao,taarifa inadai kuwa idadi ya vifo imeongezeka.
Na Hobokela Lwinga
Idadi ya vifo katika ajali iliyotokea jana Juni 5, 2024 imeongezeka kufikia watu 16, huku miili minane ikitambuliwa na majeruhi wengine wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Ajali hiyo iliyotokea katika mteremko wa Simike, eneo la Mbembela lilihusisha lori ambalo lilifeli breki na kugonga magari mawili, ikiwamo Coaster iliyokuwa na abiria ikitokea Tunduma mkoani Songwe.
Ilielezwa wakati lori hilo likiteremka katika mlima huo, lilifeli breki na kugonga gari dogo, kisha kuigonga Coaster iliyokuwa imesimama eneo la Mbembela. Pia iligonga bajaji, pikipiki na guta na kusababisha vifo vya watu 13 na majeruhi 18.
Akizungumza na kituo hiki Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo Petro Seme amesema jana walipokea jumla ya watu 22, ambapo kati yao 14 walikuwa wamefariki na wengine majeruhi.
Amesema katika majeruhi hao, wawili wamefariki wakati wakiendelea na matibabu, akieleza kuwa jopo la madaktari wanaendelea kutoa huduma kwa maheruhi wakiwamo watatu waliokuwa katika uangalizi maalumu.
