Baraka FM
Baraka FM
12 May 2026, 08:26

Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mbozi kwamara ya kwanza wamepata Askofu kiongozi katika jimbo hilo Mchungaji Julius Sikana.
Na Hobokela Lwinga
Jamii yaaswa kutokuwa na roho ya kisasi badala yake wawe na roho ya msamaha.
Askofu Mteule wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mbozi, Mchungaji Julius Sikana, amesimikwa rasmi kuwa Askofu wa kwanza wa jimbo hilo katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini pamoja na serikali.

Hafla hiyo ya kihistoria imefanyika katika viwanja vya TACRI vilivyopo vwawa Mkoa Wa Songwe huku viongozi wa kanisa wakisisitiza mshikamano, upendo na kuendelea kuhubiri Injili kwa jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Mchungaji Conrad Nguvu Mali, aliwataka Wakristo kudumisha moyo wa kusameheana pamoja na kuendelea kueneza Injili kwa watu wote ili kujenga jamii yenye maadili mema.

Kwa upande wake, Askofu mpya wa Jimbo la Mbozi, Mchungaji Julius Sikana, aliishukuru serikali kwa ushirikiano wake na kuomba kusaidiwa kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii pamoja na jimbo hilo, ikiwemo kuboresha miundombinu na kuongeza fursa za ajira katika miradi inayosimamiwa na kanisa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Makame, aliyemwakilisha mgeni rasmi Rais Samia Suluhu Hassan, alisema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini na kuahidi kufanyia kazi changamoto zilizowasilishwa ambazo zinawezekana kupatiwa ufumbuzi.

Kwa upande mwingine, Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Mchungaji Robert Pangani, aliahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa askofu huyo mpya katika utekelezaji wa majukumu yake ya kiroho na kijamii.

Jimbo la Moravian Mbozi limeanzishwa kutoka Jimbo la Kusini Magharibi ambalo hapo awali lilikuwa chini ya uangalizi wa Askofu Robert Pangani, na sasa linaongozwa rasmi na Askofu wake wa kwanza, Mchungaji Julius Sikana.