Baraka FM
Baraka FM
17 June 2026, 11:46

Kampuni ya Tanzania Innovation and Creative Opportunities Network (TICON) imezindua kampeni maalumu ya kuhamasisha wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Mbeya kushiriki katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo mkoani humo, kwa lengo la kuongeza uelewa na kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi.
Na Ezra Mwilwa
Kutokana na uwepo wa vivutio vingi vya utalii mkoani Mbeya, uongozi wa Kampuni ya Tanzania Innovation and Creative Opportunities Network (TICON) umezindua mpango mkakati wa kutangaza maeneo mbalimbali ya utalii yaliyopo mkoani humo kupitia mashindano yatakayowashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu.
Akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Jiji la Mbeya, Bi. Anna Joseph, ameipongeza TICON kwa kuandaa tukio hilo, akieleza kuwa itasaidia kutangaza utalii wa ndani pamoja na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu rasilimali zilizopo mkoani Mbeya.
Bi. Anna amesema Halmashauri ya Jiji la Mbeya itaendelea kutoa ushirikiano katika kila hatua ya utekelezaji wa kampeni hiyo ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.
Kwa upande wao, viongozi wa TICON, Mkurugenzi Aman George na Katibu wa kampuni hiyo,Liveti Japhet, wamesema wameamua kuanza kampeni ya utangazaji wa vivutio vya utalii kupitia vijana wa vyuo vikuu kwa kuwa wana uwezo mkubwa wa kutumia majukwaa ya kidijitali kufikisha ujumbe kwa jamii.
Wameongeza kuwa baada ya hatua hiyo, kampeni itapanuliwa na kuwafikia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi kutoka vyuo vitakavyoshiriki, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chison Munga,amesema wamepokea kampeni hiyo kwa mikono miwili na kuahidi kushiriki kikamilifu katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Mbeya.
Naye Happiness Fulumisi amesema mchakato wa kumpata mshindi wa mashindano hayo utahusisha upigaji kura, ambapo kila kura itagharimu shilingi 500 za Kitanzania.
Mashindano hayo yalianza Juni 1, 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 30, 2026, yakibebwa na kaulimbiu isemayo: “Tanzania Yetu, Tuisimulie Sisi Wenyewe.”