Baraka FM

Biteko aridhishwa ujenzi wa miradi ya umeme

20 February 2024, 16:08

Na Hobokela Lwinga

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Dotto Biteko amefanya ziara leo tarehe 20.2.2024 na kukagua miradi ya uendelezaji wa umeme wa joto ardhi katika eneo la Kyejo Mbaka pamoja na Ngosi ikiwa ni hatua ya kuongeza upatikanaji wa umeme nchini Tanzania.

Mhe. Biteko ameridhishwa na kiwango cha ujenzi kilichofikiwa na kuwa miradi hii itakapokamilika itaongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini na hivyo kuongeza kiwango cha uchumi kwa wananchi.

Mradi wa Kyejo (Busokelo)unatarajia kuzalisha kiwango cha megawati 60 huku Ngosi iliyopo kata ya Isongole (Rungwe) ikitoa Megawati 70

Mhe. Biteko amewatoa hofu watanzania dhidi ya kukatika katika kwa umeme na kuwa hali hii inatokana na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme ambapo kwa sasa hatua nzuri imefikiwa huku Mashine zikianza kufungwa katika Bwawa la Nyerere ambalo litaondoa adha yote ya uhaba wa umeme nchini.

Aidha ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mingine ya umeme kama ,gesi, pamoja upepo ambayo yote kwa pamoja itaongeza upatikanaji wa umeme hasa vijijini ambako umeme umepelekwa kuchavusha uchumi wa wananchi kupitia Mpango wa REA.

Katika hatua nyingine amewahimiza Wakazi wa Wilaya ya Rungwe kujitokeza kwa wingi katika zoezi la Uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, huku wakidumisha amani na utulivu silaha waliyotuachia waasisi wa taifa hili.

UMEME WA JOTO ARDHI NI NINI?

Huu ni umeme unaotokana na joto lililopo ardhini ambalo huchimbwa katika kina kirefu katikati ya miamba (core) ambalo hupandishwa ardhini na hivyo kusaidia upatikanaji wa umeme.

Umeme huu hupatikana katika maeneo ambayo yamepitiwa na bonde la Ufa.

Miradi kama hii inatekelezwa eneo la Songwe lililopo Mbozi Songwe ambalo watafiti wanaonesha kuwa ndiyo mkondo mmoja pamoja na Ngosi na Kiejo Mbaka.