Baraka FM

Serikali yaombwa kuharakisha ujenzi wa daraja Chunya

9 November 2023, 14:55

Na mwandishi wetu

Wanachi wa vijiji Lualaje na Mwiji kata ya Lualaje halmashauri ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa daraja la Lualaje linalounganisha kata hiyo na Mapogolo wilaya ya Chunya kabla ya msimu wa mvua kuanza ili kuwarahisishia usafarishaji wa pembejeo za kilimo na mazao kutoka mashambani. 

Yusuph Mwangoka, kijana kutoka kata hiyo amesema wanaishukuru serikali kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni mia mbili kwa ajili ya ujenzi huo wa daraja na likikamilika litapunguza adha ya usafiri na usafrishaji wa mazao, pembejeo na abiria kuelekea barabara kuu ya Mbeya Tabora.

Mwangoka amesema kwa hivi sasa wanatumia gharama kubwa kusafirisha mazao ya mashambani, pembejeo za kilimo na bidhaa za madukani.

“Kama ulivyoona kata yetu wananchi ni wakulima hivyo ujenzi wa daraja hili ambalo linaunganisha kata ya Lualaje na kata ya Mapogolo hivyo kukamilka kutapunguza gharama za uzalishaji na kumpa nafuu mwananchi wa kawaida, cha msingi tunaomba likamilishwe kwa wakati kabla ya mvua hazijaanza” anasema Mwangoka.

Ameongeza kuwa wananchi katika kata hizo wanajishughulisha na kilimo cha tumbaku na mtumba mmoja wa tumbaku wanasafrisha kwa shilingi 5,000/= lakini daraja likikamilika gharama zitapungua hadi kufikia shiling 1,400/= kutoka shambani kwenda kwenye maghala hivyo wanaiomba serikali imlipe mkandarasi haraka ili aweze kukamilsha ujenzi wa daraja hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Comrade Juma Homera amemtaka mkandarasi kufanya haraka ukamilishwaji wa daraja hilo ambalo ni tumaini kwa wasafirisha mazao na wanafunzi ambao wanategemea daraja hilo kuvuka kuwahi masomo shuleni.

“Kama unavyofahamu maji yakijaa pale hakuna mwanafunzi wala mtoto atakayepita hapo kwahiyo naomba uongozi wa kijiji na kata mbali na mkandarasi kufanya haraka ukamilishwaji wa daraja hili lakini pia nyie msaidieni mkandarasi vifaa vyake visiibwe.”