Baraka FM

Mamba mla watu auawa Mtera Iringa

14 January 2024, 20:01

Na Moses Mbwambo, Iringa

Hivi karibuni Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego, Kuingia kazini kusaka Mamba leo Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania Tawa kwa Kushirikiana na Wananchi wa Kata ya Migoli Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wamefanikiwa kumuua Mamba mmoja katika bwawa la Mtera Mwalo wa Mapropeller

Akizungumza na Wanahabari Kaimu Kamishina wa TAWA kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Martha Msemo amesema kuwa kuvuliwa kwa mamba hao ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Dendego kuruhusu kutumia silaha za asili ambazo ndizo zimefanikisha kuuawa kwa miongoni mwa mamba mmoja ambao wamekuwa ni wakorofi katika Bwawa hilo.

Pia Msemo amesema kuwa baada ya kuingia kazini walitega mtego wa ndoano iliyowekwa nyama ya Mbwa ndio iliyofanikisha kumnasa mamba huyo na wao bado wapo kazini kuendelea kuwasaka mamba wale ambao ni wasumbufu ili kuwasaidia wavuvi wasiweze kukumbwa na changamoto hiyo ya kuliwa na mamba wawapo katika shughuli zao za uvuvi

Nao baadhi ya wavuvi wameishukuru serikali kwa jitihada kubwa walioionesha baada ya haya majanga yaliyowakumba hivi karibuni na kuiomba serikali kuweza kuwapatia mikopo ili waweze kupata vifaa vya kisasa vitakavyowasaidia kwenye shughuli.

Wavuvi Zaidi ya wane wameuawa na mamba wakati wakivua samaki katika Bwawa hilo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita