Baraka FM

Kamanda wa polisi Songwe apandishwa cheo

21 February 2024, 14:46

Namwandishi wetu, Songwe

Maofisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wa Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoani Songwe wakiongozwa na Afisa Mnadhimu, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP GALLUS HYERA wamempongeza Kamanda wa Polisi Mkoa huo kwa kupandishwa cheo kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi hadi kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi.

Akitoa Pongezi hizo kwa niaba ya askari Afisa Mnadhimu ACP HYERA amebainisha kuwa, kitendo cha Kamanda huyo kupandishwa cheo na Mheshimiwa Rais ni kuaminiwa na kuonesha utendaji kazi mzuri ndani ya Mkoa huo ambao ni lango la SADC.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Theopista Mallya akizungumza na askari aliwapongeza wananchi ambao wanaendelea kufuata sheria na kuufanya Mkoa wa Songwe kuwa shwari ukiachana na wale wachache ambao bado Jeshi la Polisi linaendelea kutoa elimu ili kila mmoja aache uhalifu na jamii iwe salama.

Pia alimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia upandishwaji huo lakini pia alimshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Camillus Wambura ikiwa ni pamoja na kuwashukuru Askari wote wa Mkoa wa Songwe kwa kumpa ushirikiano mzuri wa kutekeleza majukumu ya kazi za Polisi na kuwataka waendele kutekeleza majukumu ya Jeshi la Polisi kwa kuzingatia Kauli mbiu ya Jeshi la Polisi.

Pongezi hizo pia ziliambatana na hafla ya ukataji wa keki iliyoandaliwa na askari wa Mkoa wa Songwe.