Baraka FM
Baraka FM
4 April 2026, 07:38

Askofu Pangani ahimiza jamii kuzingatia maadili mema, mshikamano na hofu ya Mungu ili kujenga taifa lenye amani na ustawi.
Na Hobokela Lwinga
Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Robert Pangani, amewahimiza Wakristo nchini kutumia kipindi cha tafakari ya kifo cha Yesu Kristo kama fursa ya kuacha kutenda maovu na kuishi maisha yanayoendana na mapenzi ya Mungu.

Rai hiyo ameitoa wakati wa Ibada 8 ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi, Ushirika wa Yeriko, uliopo katika Halmashauri ya Mji Mdogo wa Mbalizi, mkoani Mbeya.

Askofu Pangani amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Wakristo kuendelea kujiungamanisha na Mungu nyakati zote ili waweze kufikia mafanikio ya kiroho na kimwili.

Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kuliombea taifa lao ili kudumisha amani, ambayo imekuwa ni tunu na desturi ya nchi.

Katika hatua nyingine, Askofu huyo amewakumbusha wazazi na walezi umuhimu wa kutoa malezi bora kwa watoto wao,Amekemea vikali tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kuwafukuza nyumbani mabinti wanaopata ujauzito wakiwa bado chini ya uangalizi wao, akieleza kuwa hali hiyo huchangia kuongezeka kwa watoto wa mitaani na hatimaye kusababisha ongezeko la uhalifu katika jamii.