Baraka FM
Baraka FM
3 June 2026, 21:07

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za kijamii kwa kuwekeza katika vituo vya ESRACS ili kuboresha utambuzi wa mapema na huduma za watoto wenye mahitaji maalumu nchini.
Na Hobokela Lwinga
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Maulid Hassan Sulumbu, amesema Serikali inaendelea kuweka msisitizo katika kuboresha huduma za kijamii nchini, hususan sekta za elimu, afya na ustawi wa watoto, ili kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa za maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Ujenzi na Matumizi ya Vituo vya Utambuzi na Upimaji wa Watoto (ESRACS), uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya, Sulumbu amesema uwekezaji katika vituo hivyo ni hatua muhimu ya kuimarisha elimu jumuishi na huduma kwa watoto wenye mahitaji maalumu,Kampeni hiyo inaratibiwa na HakiElimu kwa ushirikiano na Child Support Tanzania.
Aidha, amesema kuwa kati ya halmashauri 184 zilizopo nchini, ni halmashauri 36 pekee ambazo hadi sasa zina vituo vya ESRACS, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuongeza juhudi za kusambaza huduma hizo katika maeneo mengi zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Tanzania, Mary Ndaro, amesema changamoto kubwa inayoikabili sekta hiyo kwa sasa ni uchache wa vituo vya utambuzi na upimaji wa watoto,Amesema kuongezeka kwa vituo hivyo kutasaidia kuboresha huduma za utambuzi wa mapema na upimaji kwa watoto wenye mahitaji maalumu, hatua itakayowezesha kupata msaada stahiki kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Child Support Tanzania, Noela Msuya, amesema uwepo wa kituo cha ESRACS katika Shule ya Msingi Mwenge umewezesha watoto wengi kutambuliwa mapema na kupatiwa msaada unaohitajika mara baada ya kubainika kuwa na ulemavu au changamoto za maendeleo.

Mmoja wa wazazi walionufaika na huduma hizo amesema upimaji wa mtoto wake ulimsaidia kutambua mahitaji maalumu ya mtoto huyo na kupata mwongozo wa namna ya kumsaidia, hali ambayo imechangia mtoto kuendelea na masomo yake bila changamoto kubwa.
Uzinduzi huo umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Utambuzi wa Mapema, Msingi wa Elimu Jumuishi na Bora kwa Watoto Wote.”