Baraka FM

Tengeni maeneo ya kujenga miundombinu ya maendeleo kwenye maeneo yenu

12 January 2024, 18:02

Na mwandishi wetu,Chunya

Kamati ya fedha, Uchumi na Mipango ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya ikiongozwa na Makamu mwenyekiyi wa Halmashauri imeagiza viongzoi wa vijiji na kata zote kutenga maeneo ya kujenga miundombinu ya maendeleo katika vijiji na kata zao ili kuepuka kutumia fedha za mradi kulipa fidia pindi mradi utakapoanza kujengwa.

Hayo yametolewa wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Kambikatoto ambayo tayari imeshanaza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza ambapo wanafunzi 88 wamepangwa kuripoti katika shule hiyo kwa mwaka wa masomo 2024.

Akitoa maoni wakati wa ziara hiyo makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Mhe Ramadhani Shumbi amesema haiwezekani kutumia fedha zilizotengwa kwaajili ya mradi Fulani kuanza kutumika kulipa fidia watu wenye maeneo wakati serikali ina maeneo makubwa kuliko wananchi wakawaida.

“Haiwezekani milioni tatu na laki tatu kutumika kuwalipa fidia wananchi ili kupisha eneo la kujenga shule maeneo ya vijijini kama Kambikatoto kwani fedha hizo zingetumika kwaajili ya kuendeleza mambo mengine ambayo ni muhimu sasa ni lazima viongozi wa vijiji na kata kutenga maeneo yatakayotumika kujenga miradi ya maendeleo hii ya kulipa fidia haitakiwi kuwepo kwa maeneo kama haya ya wilaya yetu” Alisema Mhe Shumbi.

Mhe Sailon Mbalawata diwani wa kata ya Bwawani na mjumbe wa kamati hiyo ameshauri viongozi wa kata kuhakikisha eneo la shule lenye ukubwa wa hekari 21.5 linahifadhi vizuri kwa kuhakikisha hati zake zinapatika kwa wakati kwani kuchelewa kufanya hivyo inaweza kuleta usumbufu usio wa lazima hapo baadaye.

Aidha wajumbe wa kamati wameshauri viongozi wa kata hiyo kuongeza juhdi kuhakikisha wanafunzi wote waliopangwa kuripoti shule wanaripoti haraka iwezekanavyo hadi kufikia tarehe 25/1/2024 wanafunzi wote wawe wemeripoti tayari kuanza muhula wa masomo kama serikali inavyotaka.

Jengo la utawala la shule ya sekondary kambikatoto wilayani chunya mkoa wa Mbeya

Kamati ya Fedha, uchumi na Mipango iko katika siku ya kwanza ya ziara yake na imetembelea na kukagua miradi yenye thamani ya shilingi 697,180,000/= ambayo ni pamoja na Mradi wa ujenzi wa Shule ya sekondari kambikatoto iliyopewa shilingi milioni mia tano na themanini na tatu (583, 180,000/=), mradi wa ukamilishaji wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo shule ya sekondari Bitimanyanga ambayo ilipewa shilingi milioni thelasini na moja (31,000,000/=) pamoja na mradi wa Ujenzi wa Shule shikizi ya msingi Tulieni iliyopewa shilingi milioni themanini na tatu (83,000,000/=)