Baraka FM

Jamii yatakiwa kuondokana  na imani potofu

28 December 2023, 18:20

na Mwandishi wetu,Songwe

Wanakijiji wa kijiji ya Hangomba wilayani Mbozi wametakiwa kuachana na imani potofu za kishirikina ikiwemo ramli chonganishi pamoja na unywaji wa pombe uliopindukia.

Kauli hiyo imetolewa Disemba 17, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya wakati akizungumza na wanakijiji hao kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu madhara ya kujichukulia sheria mkononi na kusababisha mauaji pamoja na vitendo vingine vya kikatili

Kamanda Mallya alisema kuwa, unywaji Pombe kupindukia umekuwa na matokeo hasi kwenye jamii ambapo asilimia kubwa ya watu waliojiingiza kwenye matendo hayo wamekuwa wakiishia kwenye mikono ya sheria baada ya kutenda matendo yaliyokinyume na sheria, kanuni na taratibu za nchi.

“Unapo kunywa pombe kupita kiasi au unapokuwa mtu wa kuamini imani potofu za kishirikina na ramli chonganishi ni lazima utafanya vitendo viovu, kinachotakiwa ni kumrudia Mwenyezi Mungu na kuacha kabisa vitendo hivyo ili kuepuka kuingia kwenye mkono wa sheria”. Alisema Kamanda Mallya

Kamanda Mallya alihitimisha kwa kutoa wito kwa wanakijiji hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe ili kudhibiti matukio ya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina na uhalifu mwingine kwenye maeneo yao.