Baraka FM

Zaidi ya miche 100 yapandwa shule ya Mpakani Kyela

29 February 2024, 18:51

Na Ezekiel Kamanga

Taasisi ya Living Together Youth Foundation(LTYF) yenye makao makuu wilaya ya Kyela inayojihusisha na utunzaji wa mazingira ikiongozwa na mkurugenzi wake Leonatha Likalango imeendelea na kampeni ya kufungua klabu za mazingira shuleni sanjari na upandaji miti ya matunda na vivuli katika maeneo ya shule, taasisi za umma na binafsi lengo likiwa ni kuhifadhi mazingira pia kujipatia lishe kutokana na matunda pamoja na kujiongezea kipato na kupata vifaa vya ujenzi.

Akizindua klabu ya mazingira na kuendesha zoezi la upandaji miche zaidi ya mia shule ya mchepuo wa kiingereza ya Mpakani Likalango amesema watoto wakipewa elimu ya mazingira watakuwa mabalozi wazuri kwani elimu hiyo wataifikisha kwa wazazi wao nyumbani.

Aidha shule hiyo ni mpya na haina miti ya matunda na vivuli hivyo miti hiyo itasaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo,kuzuia upepo,kuwapatia matunda kwa watoto na kuifanya shule iwe na mandhali nzuri ya kuvutia.

Changamoto ya taasisi hiyo changa ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa mbegu za miti pamoja viriba kwa ajili ya uoteshaji miti ili zoezi hili liifikie nchi nzima kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele kupambana na uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Vitalis Mlambia Mwalimu mkuu shule ya Mpakani ameishukuru taasisi ya Living Together Youth Foundation kwa uzinduzi wa klabu na kuendesha zoezi la upandaji miti.

“Naahidi kuisimamia miti iliyopandwa ili itunzwe vizuri na kila mtoto amepanda mti wake ambao atautunza kipindi chote atakachokuwa shuleni”alisema Mlambia.

Winfrida Goldon ni balozi wa eneo hilo ambaye ameshiriki kikamilifu zoezi la upandaji miti amesema binafsi amepata elimu ya mazingira.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kilambo Adam Mwaikono ameishukuru taasisi hiyo kuendesha zoezi hilo ambalo limekuwa na tija kwenye kitongoji chake.

Bryson Alex Mwenyekiti wa shule na Ayoub Mwakabanga Makamu Mwenyekiti wa shule hiyo wameahidi kuitunza miti hiyo ili kuhakikisha miti iliyopandwa inakua vema.

Likalango amesema taasisi yake haishii kuzindua klabu na upandaji miti tu bali hufuatilia maendeleo ya klabu na miti iliyopandwa kama ilivyofanyika katika shule ya msingi Kilambo ambayo ilizindua klabu ya mazingira septemba 8,2023 wakati wa mbio za mwenge wa uhuru.

Mwalimu Devota Sanga ni mlezi wa klabu ya shule ya msingi Kilambo amesema miti yote iliyopandwa mwaka jana kwenye mbio za mwenge inaendelea vizuri na watoto wanaipenda klabu yao ya mazingira ambapo kila mtoto anaufurahia mmea wake aliokabidhiwa kuutunza.

Baadhi ya wanafunzi Esther Patrick,Neema Jackson,Patrica Frank,Stekela Panja na Meshack Makumbusho wamesema kila wakifika shule huhakikisha wanaiangalia miti yao na kuifanyia palizi na umwagiliaji mara kwa mara ili isikauke.

Pia wameelezea faida za miti ni kuwapatia hewa safi pamoja na vivuli.

Miti iliyopandwa ni pamoja na mijohoro kwa ajili ya kivuli na milimao kwa ajili ya matunda ambayo itawasaidia kuongeza kipato katika shule.

Katika hatua nyingine meneja wa taasisi ya Living Together Youth Foundation Noel Kayombo amesema wajibu wake ni kubaini maeneo yenye changamoto ya mazingira ili kuhakikisha nchi nzima inafikiwa na elimu ya utunzaji wa mazingira kwa kuhakikisha jamii inapanda miti pia kuacha utupaji hovyo wa chupa za maji na vinywaji.

Hivi karibuni taasisi itafanya zoezi la upandaji miti makao makuu ya Polisi Wilaya ya Kyela ukiwa ni mwendelezo wa kutunza mazingira na vyanzo vya maji.