Baraka FM

Nyimbo za chadema zakwamisha mkutano wa Mwabukusi, aitwa na jeshi la polisi Mbeya kujieleza

11 October 2023, 16:34

Wakili Boniface Mwabukusi akiwa katika ofisi za jeshi la polisi mkoa wa Mbeya zilizopo kata ya Forest jijini Mbeya (Picha na Josea Sinkala)

Kila nchi ina utaratibu wake katika kujiongoza, Tanzania ni moja ya nchi inayoongozwa kwa mujibu sheria kupitia katiba ya nchi na katika hali hiyo hakuna mtu ambaye yupo juu ya sheria hivyo kila mtu anapaswa kutii na kuheshimu uwepo wa katiba.

Na Josea Sinkala

Wakili wa kujitegemea Boniface Mwabukusi amefika mbele ya Jeshi la Polisi makao makuu mkoa wa Mbeya na kuhojiwa juu ya tuhuma za kufanya kusanyiko lisilo halali huko Busokelo wilayani Rungwe mwishoni mwa juma lililopita.

Wakili Mwabukusi amekiambia kituo hiki kuwa aliitwa na polisi (Oktoba 09, 2023) lakini aliahidi kwenda (Oktoba 10, 2023) ambapo amehojiwa na kutoa maelezo yake kuhusu kufanya kusanyiko lisilo halali.

Amesema alipofika polisi aliandika taarifa zake binafsi na hakuna taarifa zozote alizotoa zaidi.

Aidha Wakili Boniface Mwabukusi amesema baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa na Jeshi la Polisi aliachiwa kwenda kuendelea na majukumu yake hadi baadaye baada ya majuma mawili ambapo ataripoti Polisi.

Sauti ya Wakili Boniface Mwabukusi

Naye Wakili wa kujitegemea Philip Mwakilima amesema Balozi mstaafu Dkt. Wilbroad Slaa pamoja na Mwenyekiti mtendaji wa Mtandao wa TRAFO Buberwa Kaiza ambao walishikiliwa tangu Oktoba 09, 2023 nao wakihusishwa na tuhuma za kufanya mkutano usio halali walihojiwa na kumaliza mahojiano yao majira ya saa moja usiku wa (Okt.09, 2023).

Wakili Mwakilima anasema pia Buberwa na Dkt. Slaa watatakiwa kuripoti Polisi baada ya majuma mawili huku taarifa kuhusu mwanaharakati Mdude Mpaluka Nyagali zikidai kuwa hajaenda polisi tangu alipoitwa Oktoba 09, 2023 akidaiwa kuhusishwa kwenye tuhuma hizo.

Wakati hayo yakiendelea Mdude ambaye ni mratibu wa maandamano ya amani ya kupinga mkataba wa bandari na kudai katiba mpya, amesisitiza kupitia waraka wake hivi karibuni azma ya kuendelea kuratibu maandamano hayo anayodai yatazinduliwa jijini Mbeya Novemba 09, 2023.