Baraka FM

Askofu Mwakijambile azikwa kijijini Isaki Kyela

12 December 2024, 09:32

Dunia ni njia ya kupita wengi lakini katika upitaji wa dunia hakuna ambaye anajua siku ya kumaliza safari yake duniani hivyo tuishi maisha ya uchaji kwa Mungu.

Na Kelvin Lameck

Waumini wa madhehebu mbalimbali nchini wametakiwa kuheshimu viongozi wao wa kanisa wakiwemo Wachungaji na Maaskofu ili waendelee kufanya kazi ya Mungu kwa kueneza injili.

Hayo yamesemwa na Askofu wa Makanisa ya Brotherhood Tanzania Rabi Mwakanani wakati akihubiri katika ibada ya mazishi ya Askofu mstaafu wa kanisa la Kiinjili la Moravian Samweli Asumwisye Mwakijambile huko wilayani Kyela mkoani Mbeya.

Aidha Askofu Mwakanani amewataka viongozi wa makanisa kuishi maisha ya kumpendeza Mungu badala ya kuendekeza migogoro ambayo inaweza kurudisha nyuma kazi ya Mungu.

Askofu wa Makanisa ya Brotherhood Tanzania Rabi Mwakanani(kulia)na Askofu wa kanisa la kiinjili la Moravian Joseph Mwambungu katika ibada ya mzishi ya Askofu Samwel Asumwisye Mwakijambile

Naye Askofu wa kanisa la kiinjili la Moravian Joseph Mwambungu amewataka waumini kuendelea kuwa na umoja na mshikamano ili kuhakikisha wanaendeleza mazuri yote yaliyofanywa na marehemu Askofu Mwakijambile.

Hata hivyo viongozi mbalimbali wa kanisa la Moravian jimbo la kusini na viongozi wa kanisa la Babtist akiwemo Nielsem Mwaisango, askofu Lusekelo Mwakafwila, Mchungaji Kabigi na wengineo wametoa pole kwa kanisa kumpoteza mtu muhimu.

Askofu mstaafu kanisa la Moravian jimbo la kusini Lusekelo Mwakafwila (wa pili kulia)akishiriki ibada ya mazishi ya Askofu Samwel Asumwisye Mwakijambile

Marehemu Askofu Samwel Asumwisye Mwakijambile alizaliwa tarehe 15 juni 1936 na kufariki dunia tarehe 4 Disemba 2024 jijini Dar es salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na amezikwa nyumbani kwake Isaki Kyela.