Baraka FM

Mchungaji Mwambalaswa: utoaji wa sadaka ni sehemu muhimu ya ibada

21 July 2026, 10:56

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Mchungaji Paul Samwel Mwambalaswa. Picha na Maick Ngondo

Utoaji wa sadaka ni sehemu muhimu ya ibada na ishara ya kumshukuru Mungu kwa baraka anazotujalia.

‎‎Na Hobokela Lwinga

‎ Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Mchungaji Paul Samwel Mwambalaswa, ameongoza ibada ya harambee ya Kanisa la Moravian Wilaya ya Mbalizi iliyofanyika katika Ushirika wa ZZK, uliopo Mji Mdogo wa Mbalizi.

‎Ibada hiyo ilifanyika Jumapili, Julai 19, 2026, na kukutanisha viongozi wa kanisa, waumini pamoja na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Mbalizi.

‎Upande wa liturujia uliongozwa na Mwenyekiti wa Wilaya ya Mbalizi, Mchungaji Robert Sikanyika, huku Mchungaji Paul Samwel Mwambalaswa akitoa mahubiri yaliyowahimiza waumini kuendelea kushirikiana katika kuimarisha kazi ya Mungu na maendeleo ya kanisa.

Mwenyekiti wa Wilaya ya Mbalizi KMT -JKM Mchungaji Robert Sikanyika(picha na Maick Ngondo)

‎Viongozi wengine walioshiriki katika ibada hiyo ni wenyeviti wa wilaya mbalimbali zinazounda Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, akiwemo Mchungaji Greenwell Sinkwembe (Wilaya ya Mbeya), Mch.Paul Mwampamba (Wilaya ya Mbarali), Mchungaji Nuru Mwamahonje (Wilaya ya Chunya), Mchungaji Steven Waya (Wilaya ya Ilembo), Mchungaji Godfrey Tinga (Wilaya ya Uyole), pamoja na mwenyeji wao, Mchungaji Robert Sikanyika wa Wilaya ya Mbalizi.

Baadhi ya wenyeviti wa wilaya zinazounda KMT-JKM (picha na Maick Ngondo)

Ibada hiyo ya harambee ilihudhuriwa na waumini  pamoja na wageni mbalimbali, ambao walijitokeza kushiriki ibada na kuunga mkono jitihada za maendeleo ya Kanisa la Moravian katika Wilaya ya Mbalizi.

Baadhi ya waumini na wageni mbalimbali katika Harambee ya wilaya ya Mbalizi ushirikani ZZK(picha na Maick Ngondo)