Baraka FM

Jeshi la polisi Mbeya watembelea wagongwa

21 August 2026, 23:10

Miongoni mwa maafisa wa jeshi la polisi mkoa wa Mbeya wakiongozwa na RPC Benjamin Kuzaga(picha na Ezra Mwilwa)

Katika kujenga umoja na ushirikiano katika jamii taasisi mbalimbli nchini zimeendelea kutembelea na kutoa misaada kwa watu wasio jiweza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amewaongoza Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mbeya kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa akina mama waliolazwa Kituo cha Afya Ruanda Mwanjelwa Jijini Mbeya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga(picha na Ezra Mwilwa)

Akizungumza Agosti 21, 2026 mara baada ya kutembelea Kituo hicho, Kamanda Kuzaga amesema kuwa lengo la kufika katika kituo hicho ni kutoa msaada kwa akina mama ambao wamelazwa, kuwapatia vitu mbalimbali kama vile Sukari, Maziwa, Sabuni, Soda, Pampasi ili viweze kuwasaidia katika kipindi ambacho watakuwa Kituoni hapo.

Aidha, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Ibrahim Mhando kwa niaba ya Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia ameeleza kuwa wao kama Askari wa Kikosi hicho waliona ni vema kufika Katika Kituo cha Afya Ruanda kwa ajili ya kuwashika mkono kwa kuwapatia vitu mbalimbali wagonjwa ambao wamelazwa ili viweze kuwasaidia.

Naye, Bi. Adelina Amnaaye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ruanda – Mwanjelwa Mbeya amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kuchagua kutembelea Kituo hicho na kwa msaada walioutoa kwani vitu hivyo vitawasaidia wagonjwa ambao wamelazwa Hospitalini hapo.

Kwa upande wake, Witness Kiberenge kwa niaba ya akina mama waliolazwa Hospitalini hapo amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada wa vitu mbalimbali huku akitoa wito kwa jamii kuwakumbuka wagonjwa na watu wenye mahitaji maalum.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuelekea Maadhimisho ya miaka ishirini (20) ya Polisi Jamii, linaendelea kuyafikia makundi mbalimbali yenye uhitaji lengo likiwa ni kutoa elimu, misaada mbalimbali kwa makundi ya kijamii yenye mahitaji maalum.