Baraka FM

Tutende haki kuwahudumia watu

29 September 2026, 06:56

Haki nichachu ya maendelea katika jamii,kanisa na Taifa kwa ujumla

Na Hobokela Lwinga
‎
Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mbozi mkoani Songwe, Julias Sikana, amesema kuwa ili jamii, Kanisa na taifa liweze kustawi, ni lazima haki itendeke kwa watu wote bila ubaguzi.
‎
‎Askofu Sikana ameyasema hayo katika ibada maalumu ya kuwekwa wakfu kwa jengo la kuabudia la Ushirika wa Ihanda, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, ambapo amesisitiza kuwa kutenda haki hakupaswi kuwa jukumu la kundi fulani la watu pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja, hususan viongozi wa Kanisa, jamii na taifa kwa ujumla.
‎
‎Aidha, Askofu Sikana ametoa rai kwa jamii, Kanisa na taifa kuwa na moyo wa msamaha, akieleza kuwa msamaha ni miongoni mwa misingi muhimu ya kujenga amani, upendo na mshikamano katika jamii.
‎
‎Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa ibada hiyo, akiwemo Mchungaji wa Ushirika pamoja na waumini, wamesema kuwa kuishi maisha yasiyo ya haki mbele za Mungu ni dhambi na chukizo, hivyo jamii inapaswa kuzingatia haki na kumcha Mungu katika maisha ya kila siku.
‎
‎Katika ibada hiyo, Askofu Sikana pia ameongoza maombi maalumu ya kuwaombea wanafunzi wa Darasa la Saba wanaojiandaa kufanya mtihani wao, akiwataka wanafunzi hao kuwa na utulivu, bidii na kumtegemea Mungu katika maandalizi yao.