Baraka FM

Taasisi za umma na binafsi zatakiwa kuwashirikisha vijana katika kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira na amani

11 November 2026, 21:19

Picha ya pamoja kati ya washiriki wa mafunzo, wakufunzi,na viongozi wa shirika la LEO KESHO(picha na Hobokela Lwinga)

Kuwashirikisha vijana katika fursa za uongozi na utunzaji wa mazingira ni jambo muhimu kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Na Hobokela Lwinga

Taasisi za umma na binafsi zimetakiwa kutumia kundi la vijana kama chachu ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo utunzaji wa mazingira, uongozi bora na kudumisha amani.

Rai hiyo imetolewa na mkuu wa Divisheni ya maendeleo ya jamii wa Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe Dany Tweve,wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Leo Kesho kupitia mradi wa Dumisha Amani Awamu ya Pili, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Tweve amesema ili vijana waweze kuondokana na malalamiko na changamoto mbalimbali zinazowakabili, wanapaswa kuhamasishwa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali, ikiwemo kilimo, ili kujipatia kipato na kuchangia maendeleo ya jamii.

Sauti ya mkuu wa Divisheni ya maendeleo ya jamii wa Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe Dany Tweve

Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Shirika la Leo Kesho, Hassan Sikana, pamoja na Mratibu wa Mradi wa Dumisha Amani Awamu ya Pili, Musa Katyeka, wamesema mradi huo unalenga kuwajengea vijana uwezo na kuwapa fursa ya kushiriki katika kufanya maamuzi yanayohusu jamii zao.

Wameongeza kuwa mradi huo pia unalenga kuwawezesha vijana kutumia rasilimali za maji kama fursa ya kujipatia kipato, sambamba na kuwashirikisha katika juhudi za kulinda na kudumisha amani nchini.

Sauti za Mkurugenzi wa Shirika la Leo Kesho, Hassan Sikana na Mratibu wa Mradi wa Dumisha Amani Awamu ya Pili, Musa Katyeka

Naye Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Frank Mwashibanda, amesisitiza umuhimu wa jamii kuwasikiliza vijana, kuwapa nafasi za uongozi na kuwashirikisha katika shughuli za maendeleo, huku akiwataka kuendelea kulinda mazingira kwa kuepuka vitendo vinavyosababisha uharibifu wake.

Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Frank Mwashibanda(picha na Hobokela Lwinga)
Sauti ya Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Frank Mwashibanda

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata imewajengea uelewa zaidi kuhusu wajibu wao katika kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya vijiji vyao, huku wakilishukuru Shirika la Leo Kesho kwa kuwawezesha kupata mafunzo hayo.

Sauti za washiriki wa mafunzo

Mradi wa Dumisha Amani Awamu ya Pili unaotekelezwa na Shirika la Leo Kesho unafanyika katika vijiji 18 vilivyopo kwenye kata tatu za Msia, Ihanda na Ipunga, ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo