Baraka FM
Baraka FM
21 August 2026, 17:07

Kutokana na uwepo wa changamoto ya udumavu wa watoto kutokana na ukosefu wa lishe bora.
Na Ezra Mwilwa
Wazazi na walezi wametakiwa kufika mara kwa mara katika vituo vya afya ili kupata elimu kuhusu uandaaji wa lishe bora kwa watoto, hatua inayolenga kupunguza na hatimaye kutokomeza tatizo la udumavu kwa watoto.
Wito huo umetolewa na Silvester Julius, ambaye ni Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kutoka Kituo cha Afya Ruanda jijini Mbeya, wakati akizungumza na kituo hiki kuhusu umuhimu wa uandaaji wa lishe bora kwa watoto katika familia.
Julius amesema wazazi na walezi wanapaswa kuzingatia elimu inayotolewa na wataalamu wa afya kuhusu namna sahihi ya kuandaa chakula chenye virutubishi muhimu kwa watoto, ili kuwasaidia kukua na kuendelea vizuri kiafya.
Kwa upande wao, viongozi wa Serikali, madiwani kutoka Halmashauri ya Mbeya Vijijini Ester Mbega na Noah Shibada, pamoja na mwakilishi wa asasi za kiraia Yona Mwakatobe, wamesema wanaendelea kushirikiana kuhakikisha elimu kuhusu lishe bora inawafikia wazazi na walezi wote katika jamii.
Wamesema ushirikiano huo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto ya udumavu na kuhakikisha watoto wanapata lishe bora na yenye mahitaji muhimu kwa ukuaji wao.
Naye mmoja wa wazazi kutoka jijini Mbeya, Shida Masuba, ameeleza namna anavyoandaa chakula kwa ajili ya mtoto wake, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia aina na mchanganyiko wa vyakula vinavyofaa kwa mtoto.
Wazazi na walezi wameendelea kusisitizwa kufuata elimu na ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya kuhusu lishe ya watoto, ili kwa pamoja kukabiliana na tatizo la udumavu na kuhakikisha watoto wanakua katika afya njema.