Baraka FM
Baraka FM
12 July 2026, 23:44

Upatikanaji wa mitaji kwa vijana, utoaji mikopo na fursa za uwekezaji unawapa uwezo wa kujiajiri, kuanzisha na kupanua biashara, kuongeza uzalishaji na kufungua nafasi za ajira kwa wengine.Hatua hii huchochea ukuaji wa uchumi, hupunguza umaskini na utegemezi, huku ikiwajengea vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Na Hobokela Lwinga, Mbarali-Mbeya
Serikali kupitia Wizara ya Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana imetoa mkopo wa zaidi ya Shilingi milioni 349 kwa Kikundi cha Vijana cha Ukwavila (Ukwavila Youth Group) kinachojishughulisha na shughuli za kilimo biashara katika Kijiji cha Ukwavila, Kata ya Mapogolo, Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo kupitia Programu ya Bilioni 200 chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Waziri wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Nanauka, amesema mikopo hiyo inalenga kuwawezesha vijana kiuchumi bila kuzingatia itikadi za kisiasa wala historia ya mwombaji.

Dkt. Nanauka amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa vijana na wanawake nchini ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya uchumi.
Kwa upande wao, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbarali, Bi. Mary Mbwilo, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Mhe. Bahati Ndingo, wamewataka vijana kutumia fursa ya mikopo hiyo kwa ufanisi, kuwekeza katika shughuli zenye tija na kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Diwani wa Kata ya Mapogolo, Mhe. Meshack Kilemile, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuthamini mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji unaowawezesha kujitegemea kiuchumi.

Baadhi ya wanufaika wa Kikundi cha Vijana cha Ukwavila (Ukwavila Youth Group) wamesema mkopo huo utawasaidia kupanua shughuli zao za kilimo biashara, kuongeza ajira na kuinua kipato cha wanachama wa kikundi hicho. Aidha, waliahidi kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanarejesha mkopo kwa uaminifu na kwa wakati.

Kikundi cha Vijana cha Ukwavila kina jumla ya vijana 150 wenye viwango na taaluma mbalimbali za elimu, ambao kwa pamoja wanajihusisha na shughuli za kilimo biashara kama njia ya kujiongezea kipato na kuchangia maendeleo ya jamii.