Baraka FM
Baraka FM
17 April 2026, 22:37

Kanisa Moravian limetengeneza mpango mkakati wa kutekeleza maendeleo ya Kanisa kwa kipinidi cha miaka mitano.
Na Hobokela Lwinga
Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Askofu Robert Pangani, amewataka viongozi wa Idara ya Mipango, Uchumi na Maendeleo katika wilaya zote za kanisa kuhakikisha wanasimamia kwa umakini utekelezaji wa mipango mbalimbali yenye lengo la kuliimarisha kanisa la Mungu ikiwa ni pamoja na mpango mkakati wa 2026-2031.

Maelekezo hayo ameyatowa wakati wa kikao kazi cha idara hiyo kilichowahusisha viongozi kutoka wilaya zote zinazounda Jimbo la Kusini Magharibi,Kikao hicho kimefanyika katika makao makuu ya Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi.
Aidha, Askofu Pangani amewahimiza viongozi hao kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kutumia wataalamu wa taaluma mbalimbali waliopo katika maeneo yao.

Pia Amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kuwa na maisha ya maombi na kuziombea nafasi zao za uongozi ndani ya kanisa.
Kwa upande wao, viongozi wa Idara ya Mipango, Uchumi na Maendeleo KMT-JKM, Ndugu Esau Swila pamoja na Mchungaji Joram Mwasumbe, walieleza kuwa ni muhimu kwa viongozi hao kutambua wajibu wao katika kusimamia na kutekeleza mpango mkakati wa kanisa.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wamelishukuru kanisa kwa kuwa na mpango kazi unaolenga kuliimarisha. Aidha, wameshauri kuwepo kwa juhudi za makusudi katika kuandaa na kuendeleza rasilimali watu kuanzia ngazi ya ushirika.
