Baraka FM

Utalii Wa Matibabu Wa Nyemelea Mkoani Songwe

23 November 2023, 17:15

Na mwandishi wetu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa(MB), Amesema serikali itaendelea kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Songwe ili kuimarisha huduma za afya zikiwemo za kibingwa na kwamba itakapokamilika itachochea utalii wa tiba kwa wagonjwa kutoka mataifa jirani ya Zambia na Malawi.

Amebainisha hayo leo Novemba 23, 2023 mara baada ya kukagua na kuridhisha na huduma zinazotolewa, ikiwemo maendeleo ya ujenzi wa baadhi ya majengo yanayoendelea kujengwa katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe iliyopo eneo la Hasamba, Wilayani Mbozi na kuweka jiwe la Msingi.

Waziri Mkuu amesema kuimarishwa kwa huduma za matibabu katika hospitali hiyo ambayo tayari imeanza kutoa huduma za kibingwa katika maeneo manne kutavutia wagonjwa kutoka mataifa hayo jirani ya Malawi na Zambia kuja kupata huduma katika Hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Songwe. 

Awali akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya Rufaa Songwe (MOI), Dkt Juma Ramadhan Juma, amesema hadi kufikia sasa ujenzi wa hospitali hiyo umetumia zaidi ya sh. bilioni16, ambapo kiasi cha sh.bilioni 13 zimetumika kwa ajili ya ujenzi, hulu sh. bilioni 3.289 zimetumika katika unuuzi wa vifaa tiba.

Dkt Juma aliongeza kuwa, hospitali hiyo imeanza kutoa huduma za kibingwa katika maeneo makuu manne, ambayo ni huduma za kibingwa za macho, magonjwa ya wanawake na afya ya uzazi, huduma bingwa za magonjwa ya watoto pamoja na huduma ya dharura na ajali.

Aidha ,Dkt Juma amesema kuwa katika kipindi cha july 2022 hadi june 2023 hospitali hiyo imehudumia jumla ya wagonjwa 19,265 kati ya hao wagonjwa wa nje (OPD)17,929 na waliolazwa (IPD) ni 1336 kati ya hao kuna akina mama 695 waliojifungua salama.