Baraka FM

Wafanyakazi wanawake Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya watoa msaada wa kitanda chenye thamani ya Milioni 37

18 April 2024, 17:48

Baadhi ya watumishi wanawake wakiwa na Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji (wapili kutoka kushoto)

Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya imekuwa ikiboresha huduma zake siku hadi siku na kuifanya kuwa kimbilio katika mikoa ya Nyanda za Juu na nchi za Kusini mwa Afrika.

Na Ezekiel Kamanga

Watumishi Wanawake vitengo mbalimbali Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kupitia umoja wao wametoa kitanda cha kisasa kwa ajili ya upasuaji chenye thamani ya shilingi milioni thelathini na saba.

Mwenyekiti wa Umoja huo Stellah Nkwama amesema lengo ni kuungana na Wanawake wengine katika maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani inayofanyika mwezi machi kila mwaka.

Baadhi ya wafanyakazi wanawake wakiwa eneo la kukabidhi kitanda katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya

Katibu wa Umoja wa Wanawake ambaye pia ni Mkurugenzi wa Raslimali watu Miriam Msalale amesema wamechangishana ili kupata fedha hizo kupitia mishahara,posho na biashara zao.

Akipokea kitanda hicho Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Dkt Godlove Mbwanji mbali ya kuwashukuru Wanawake hao kwa maono makubwa amesema kitanda hicho kitapunguza changamoto za uhaba wa vitanda kwa ajili ya upasuaji na kwamba Mungu awabariki wote walioguswa kuchangia kitanda hicho huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kutoa misaada kutokana na Hospitali hiyo kuongeza vyumba.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Dkt Godlove Mbwanji(picha na Ezekiel Kamanga)

Aidha Mkuu wa ldara ya Upasuaji Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Dkt Lazaro Mboma amesema kitanda hicho cha kisasa kitaongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Naye Mkuu wa kitengo cha mifupa Dkt John Mbanga amesema awali katika upasuaji kulikuwa kunahitaji watu zaidi ya wanne kwa upasuaji wa mtu mmoja lakini kupitia kitanda hicho daktari mmoja anaweza kufanya upasuaji.

“Hiki ni kiwanda kipya na cha kisasa zaidi ambacho kitatuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi” alisema Dkt Mbanga.

Mhandisi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Salum Kashinje amesema kitanda hicho kimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa ambapo matengenezo yake ni rahisi ukilinganisha na vitanda vya awali.