Baraka FM

Polisi Songwe kuendeleza ushirikiano kwa wananchi

18 January 2024, 20:21

Na Mwandishi wetu Songwe.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari ili kuendelea kujiwekea mikakati ya kuifikia jamii kwa kuipatia elimu na kuijengea uelewa kuhusu madhara ya uhalifu.

Hayo yalibainishwa wakati wa kikao cha pamoja kati ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe na klabu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Songwe (SOPC) kilichofanyika 17 Januari 2024 katika ukumbi wa Southern Garden Hotel ambacho kilijadili utekelezaji wa maazimio waliojiwekea katika Midahalo ilifanyika mwaka jana November na Disemba 2023.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limewaahidi waandishi hao kuendelea kuwapa ushirikiano wa dhati na kuwasihi kuendelea kuzingatia maadili katika upokeaji wa taarifa na kuzidhibitisha kutoka kwa mamlaka husika kwa lengo la kufanya mizania (balance).

Katika Kikao hicho Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza ghasia Mkoa wa Songwe SSP Sija Kadogosa alitoa elimu ya usalama kwa waandishi wa habari pindi wanapokusanya taarifa katika maeneo yenye vurugu kwa lengo la kuhabarisha Umma kuhakikisha usalama wao kwanza kuliko taarifa wanayoikusanya kwani uhai ni bora kuliko hiyo taarifa na kufanya hivyo kutawaweka salama katika utekelezaji wa majukumu yao.

Koplo Magere kutoka Kitengo cha Makosa dhidi ya Mtandao alitoa elimu kwa waandishi hao maana ya makosa ya mtandao na hasara zake, sheria zinazo simamia makosa ya mtandao na adhabu zake ikiwa ni pamoja na kujiepusha na matapeli ambao wanatumia kutapeli jamii kupitia wizi huo na pindi waonapo au wanapohisi wanataka kufanyiwa hivyo watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili ziweze kushughulikiwa kwa haraka ikiwemo na kuwapeleka mahakamani.

Nae Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Songwe Stephano Simbeye alilishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa kutambua mchango wa waandishi wa habari na kuomba ushirikiano huo uwe endelevu ili jamii ya wana Songwe iendelee kuwa salama.