Baraka FM

Wananchi Makongolosi waishukru serikali kwa kupeleka huduma za upasuaji

29 February 2024, 16:52

Na mwandishi wetu

Wananchi wa Mamlaka ya mji mdogo Makongolosi wameushukuru  serikali ya awamu ya sita  inayoongozwa na Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapelekea vifaa tiba katika kituo cha afya cha Makongolosi kwani huduma nyingi zikiwepo za upasuaji walikuwa wanalazimika kuzifuata katika  hospitali  ya wilaya  hivyo kwa kuletewa vifaa hivyo huduma nyingi watazipata katika kituo hicho.

Pongezi hizo zimetolewa katika kituo cha afya cha Makongolosi kata ya Bwawani wakati walipokuwa wamekusanyika kwaajili ya kupokea vifaa tiba kutoka Bohari ya Dawa (MSD) vyenye thamani ya million 212 vilivyonunuliwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hilda Fande , Amosi Mwazembe,  wakazi wa kata ya Bwawani mamlaka ya mji mdogo Makongolosi  kwa niaba ya wananchi waliojitokeza kushuhudia mapokezi ya vifaa tiba katika kituo cha afya Makongolosi wamefurahi kwa kusogezewa huduma za afya hususani vifaa vya  upasuaji pamoja na jokofu la kuhifadhia miili ya wapendwa wao walio tangulia mbele za haki  kwasababu kipindi cha nyuma iliwalzimu kuifwata huduma hiyo katika hospitali ya Wilaya  kitu ambacho kilikuwa ni changamoto kubwa sana kwao

“Tunashukuru sana mama yetu kutusogezea huduma sisi wakinamama tulikuwa tunahangaika sana kipindi cha nyuma tulikuwa tukiondokewa na wapendwa wetu tunalazimika kupeleka Hospitali ya Wilaya ya Chunya…, Tulikuwa na changamoto kubwa kipindi cha nyuma tulikuwa  na huduma ya zahanati tu lakini kwasasa tunakituo cha afya na leo tumeletewa vifaa tiba kama jokofu la kuhifadhia miili ya wapendwa wetu wanapotutoka  tunamshukuru Mhe.Rais kwa kutujali wananchi wakei”.walisema Hilda na Amosi.