Baraka FM

RC Homera acharuka, aagiza jeshi la polisi kushughulikia wavunja amani

5 November 2023, 15:49

Mazoezi ya “Show Off” yamefanyika kwa vikosi vya Jeshi la Polisi kuzunguka Jiji la Mbeya na Mji Mdogo wa Mbalizi kwa magari na kufanya doria za miguu kuonesha umahiri wa namna ya kuzuia uhalifu na kukabiliana na hali yoyote ya tishio ya uvunjifu wa amani.

Na Hobokela Lwinga

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Comrade Juma Homera leo Novemba 04, 2023 amelitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu, mwanaharakati au mwanasiasa yeyote atakayeingilia majukumu ya Jeshi hilo.

Akizungumza kabla ya kuanza mazoezi ya mbinu za medani za kivita na “show off” katika uwanja wa mazoezi ya kijeshi wa FFU Mbeya, Mheshimiwa Homera amekemea baadhi ya wale wanaojiita wanaharakati kutumia lugha za matusi kukashfu viongozi wa nchi na wa Jeshi la Polisi kuacha mara moja na kutoa maelekezo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya kutofumbia macho vitendo hivyo.

Pia, Mheshimiwa Homera amepongeza kazi kubwa inayofanywa na vikosi vyote vya Jeshi la Polisi ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao unakuwepo na wananchi kufanya kazi zao za maendeleo bila bugudha wala wasiwasi wowote.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Comrade Juma Homera(picha na Hobokela Lwinga)
Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Comrade Juma Homera

Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga ameeleza lengo la zoezi hilo “Show Off” kuwa ni kujiweka vizuri na kufanya mapitio ya mazoezi mbalimbali ya mbinu za medani za kivita yaliyokuwa yakifanyika.

Aidha, Kamanda Kuzaga ametumia zoezi hilo la “Show Off” lililohusisha vikosi vyote vya Jeshi la Polisi kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Mbeya kuzungumza na baadhi ya wananchi kuhusiana na masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao ya makazi na biashara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga akizungumza na askali polisi katika mazoezi yao ya kawaida katika viwanja vya FFU Sabasaba Mbeya jiji.(Picha na Hobokela Lwinga)