Baraka FM

Dkt. Tulia afanya tendo la huruma kwa wakazi wa Rungwe

2 January 2024, 18:54

Na mwandishi wetu

Spika wa  Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe.Tulia Akson Mwansasu kupitia asasi isiyo ya Kiserikali ya Tulia Trust amekabidhi nyumba mbili pamoja na kiti mwendo kwa wakazi wawili wenye mahitaji maalumu katika kata ya Kisondela na Kyimo.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni sehemu ya kampeni yake ya kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum katika wilaya ya Rungwe na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla.

Awali wakazi hao licha ya kuwa na changamoto ya viungo na hivyo kushindwa kutembea lakini pia walikuwa wakiishi katika makazi duni(Nyumba ya mianzi kama inavyooneka katika picha) na hivyo kuhatarisha ustawi wa maisha yao.

Never Kasege Mkazi wa Kijiji cha Kibisi kata ya Kyimo ni moja ya watu walionufaika na  nyumba pamoja na kiti mwendo ambapo ameshukuru kwa msaada aliopewa na kwamba  utasaidia kubadilisha sura ya maisha yake.

Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya wilaya ya Rungwe Bwana Castory Makeula amepongeza kwa hatua hiyo nzuri na kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono kazi zinazofanywa na taasisi hiyo ambayo pamoja na mambo mengine imekuwa ikitoa mikopo kwa Wajasiriamali na stadi za biashara.