Baraka FM

TANROAD Songwe yakabidhiwa gari mpya kuimarisha miundombinu ya barabara

12 December 2023, 19:09

Na mwandishi wetu, Songwe

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Dkt. Francis K. Michael katika kuimarisha sekta ya miundombinu ya barabara amekabidhi gari  aina ya Toyota Landcruiser ambalo limetolewa na serikari kupitia Wizara ya Ujenzi katika ofisi ya Wakala wa Barabara Mkoa wa Songwe (Tanroad). Hatua hii inalenga kuboresha utendaji kazi wa Tanroad na kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya barabara unafanyika kwa ufanisi zaidi.

Gari hilo jipya limepokelewa na Mkuu wa Mkoa huo katika Ofisi za Tanroad zilizopo Nselewa Mbozi, ambapo tukio hilo lilifanyika mwishoni mwa juma lililopita. Katika hafla hiyo, Mhe. Dkt. Francis alieleza umuhimu wa kuwa na vifaa vya kisasa na vyenye ufanisi katika shughuli za ujenzi na ukarabati wa barabara.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mhe. Dkt. Francis alisema, “Kupokea gari hili ni sehemu ya juhudi zetu za kuhakikisha tunaimarisha miundombinu yetu ya barabara. Tunatambua umuhimu wa kuwa na vifaa vya kisasa ili kuhakikisha miradi yetu inakwenda kwa kasi na kwa ubora wa hali ya juu.”

Gari hilo aina ya Toyota Landcruiser litawezesha wafanyakazi wa Tanroad kusafiri kwa urahisi kwenye maeneo mbalimbali ya mradi, kufuatilia maendeleo, na kutoa huduma kwa haraka zaidi kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanroad Mkoa wa Songwe aliishukuru Serikali ya Mkoa kwa mchango huo muhimu na kusema kuwa gari hilo litasaidia kuboresha usimamizi wa miradi ya barabara na kufanikisha malengo ya kuimarisha miundombinu ya usafirishaji katika mkoa wa Songwe.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Dkt. Francis K. Michael