Baraka FM

Rungwe yaonya wanaotumia taarifa za watumishi kutapeli

2 January 2024, 18:13

Na mwandishi wetu

Halmashauri ya wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imesema kupitia mitandao ya kijamii na simu za mkononi kumeibuka matapeli wanaoomba taarifa za watumishi wa umma kwa malengo yanayokinzana na sheria,taratibu na kanuni za serikali.

Taarifa hiyo imetolewa na afisa kitengo cha mawasiliano serikalini wilaya ya Rungwe Noah Kibona ambapo amesema kuwa kumekuwa na watu wakitumia jina na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Ndugu Renatus Mchau pamoja na Maofisa wa idara ya Utumishi Kuhalalisha uovu huo.

Aidha Kwa nyakati tofauti Matapeli wamekuwa wakiwalaghai watumishi kuwa watawasaidia kupanda Madaraja, Uhamisho, kuwarekebishia taarifa za utumishi na wakati mwingine kuwatishia kuwa wakishindwa kutoa ushirikiano watasitisha ajira zao.

Amesema Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe iliyopo Mkabala na Benki ya NMB imekuwa ikifuata taratibu zote kuhakikisha maslahi ya mtumishi pamoja ustawi wake yanalindwa kwa maendeleo ya taifa letu.

Kufikia hilo Idara ya utumishi imekuwa ikiyafanyia kazi Maslahi ya watumishi wake kwa kutumia kanzi data iliyopo na wakati mwingine huwafikia watumishi katika maeneo yao ya kazi kwa lengo la kutoa elimu sambamba na upatikanaji wa taarifa sahihi za mtumishi.

Hata hivyo amewakumbusha  Watumishi wote kuepuka kutoa taarifa za utumishi au eneo lako la kazi kwa mtu asiye sahihi kwani kufanya hivyo kunakinzana na Sheria pamoja na Utaratibu wa utumishi wa umma.