Baraka FM

Moravian Tanzania yarejeshewa viwanja vyake vya Dodoma

28 November 2023, 19:49

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amemuagiza Katibu Mkuu Wizara yake Eng. Anthony Sanga kuwasimamisha kazi Wapima Ardhi Enock Katete na Cleoface Ngoye kwa tuhuma za kuidhinisha na kubadilisha ramani ya eneo linalomilikiwa na Kanisa la Morovian kiwanja namba 1,2 na 3 Block T Mtaa wa Itega Jijini Dodoma.

Waziri Silaa amechukua hatua hiyo baada ya kufika eneo la tukio na kujionea hali halisi ya eneo hilo ambalo tayari baadhi ya sehemu zake tayari zimeendelezwa na kuwa na majengo ya kisasa na hivyo kumuagiza Kamishna wa Ardhi wa jiji la Dodoma Bw. Jabiri Singano kuwapa notisi ya kuhama eneo hilo wale wote waliomilikishwa eneo hilo kimakosa.

Waziri Silaa amesema baadhi ya Watendaji wa Sekta ya Ardhi wasiokuwa wema wamekuwa wakiwahonga baadhi ya Viongozi kwa kuwapa viwanja kama kinga yao mara wanapokutwa na makosa ili hali Viongozi hao wanakuwa hawana taarifa kama Watendaji hao wana nia ovu.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa (katikati)akiwa na katibu mkuu kanisa la Moravian Tanzania mch.david Mgombele(kulia),picha na mwandishi wetu
sauti za Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa na katibu mkuu kanisa la Moravian Tanzania mch.david Mgombele

Waziri Silaa amesema aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru anahusika kwa kiasi kikubwa na dhuluma za viwanja Jijini Dodoma makosa aliyoyatenda kwa kutumia cheo chake kama Mkurugenzi wa Jijiji au yeye binafsi kama Mafuru kudhulumu haki za wengine.

‘’Kuna wakati Wakurugenzi wa Mamlaka za upangaji na Watendaji Wizarani ambao wamekuwa wakipima viwanja kwa Watu wenye nguvu na kuacha kumpimia ardhi ambaye hana nguvu, katika uongozi wangu kama Waziri mwenye dhamana nitaweka mstari uliyonyooka na sitoshiriki katika dhambi kama hii”