Baraka FM
Baraka FM
1 October 2026, 12:19

Mvua za el nino ni mvua zinazoweza kuwa na athari kubwa,wananchi wanashauriwa kuendelea kuchukua tahadhari
Na Ezra Mwilwa
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya limeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa wakati wa msimu wa mvua za El Niño, hususan kuhusu usalama wakati wa mafuriko na maji kujaa.
Katika kuendeleza kampeni hiyo ya uelimishaji, Afisa Habari Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya, Sajenti Ester Kinyaga, amekutana na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mponja iliyopo katika kata ya Igawilo Halmashauri ya Jiji la Mbeya na kuwapatia elimu kuhusu namna ya kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza baada ya mvua kubwa kunyesha.
Sajenti Kinyaga amewafundisha wanafunzi umuhimu wa kuchukua tahadhari wanapokutana na maeneo yenye maji, ikiwemo namna ya kutathmini kina cha maji kabla ya kuvuka, pamoja na kuepuka maeneo hatarishi wakati wa mvua na mafuriko.
Aidha,amewafahamisha wanafunzi baadhi ya majukumu yanayotekelezwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,ikiwemo shughuli za uokoaji na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na majanga.
Akizungumza baada ya elimu hiyo, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mponja, Patrick Robert, amelishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuwafikia wanafunzi na makundi mbalimbali katika jamii ili kuwapatia elimu ya kukabiliana na majanga.

Nao baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mponja wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kufahamu hatua muhimu wanazopaswa kuchukua ili kujilinda wao wenyewe pamoja na kuwasaidia wengine wakati wa mvua hizo.
Elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya kuendelea kuelimisha jamii kuhusu tahadhari za majanga na namna ya kuchukua hatua za haraka wakati wa dharura.